Dunia ya Ughaibuni: Usawiri wa Mfalme Sulemani katika Fantasia ya Adili na Nduguze ya Shaaban Robert

Authors

DOI:

https://doi.org/10.61538/huria.v33i1.1958

Keywords:

Fantasia, Mfalme Sulemani, Uhalisiafifi, Dunia ya Ughaibuni

Abstract

Shaaban Robert amepewa sifa na hata kukosolewa juu ya utunzi wa baadhi ya riwaya zake za utanzu wa kifantasia kuwa zina mwelekeo wa kukwepa ukweli na kutia chumvi, zinasifa za kukiuka uhalisia na huwaaminisha wasomaji katika mambo yasiyo ya kawaida. Moja ya kazi hiyo ni Adili na Nduguze inayoelezewa kuwa imechanganya ‘jusura na fantasia’. Ni riwaya inayochukuliwa kuwa inakiuka kaida au mviringo wa maisha ya ulimwengu halisi.  Hata hivyo sifa za riwaya kama hizo, kupitia mkabala wa uhalisiafifi (surrealism) wa Andre Breton, ni kazi zinazochukuliwa kuwa zina uthubutu, zinazompa mwandishi uhuru wa kujieleza bila kujali mipaka ya tajriba zilizozoeleka katika jamii yake. Hivyo, makala hii inachunguza usawiri wa Mfalme Suleimani katika fantasia ya Adili na Nduguze. Lengo la makala hii ni kubainisha fikra za ughaibu katika jamii ya Waswahili kupitia kisa cha Mfalme Suleiman na kubainisha athari ya mitholojia za kidini katika Uandishi wa Robert kupitia kisa cha Mfalme/Nabii Sulemani. Data za makala hii zilikusanywa kwa kutumia mbinu ya usomaji makini na kuchambuliwa kwa kutumia mkabala wa kimaelezo. Aidha, nadharia ya uhalisiafifi imetumika katika kuchunguza, kuchambua na kuwasilisha data na matokeo ya utafiti huu. Kwa hiyo, makala hii inachanganua na kujenga hoja kwamba riwaya ya Adili na Nduguze ni kazi ya kifantansia ambayo imechota uajabuajabu kutoka katika hazina ya mitholojia na visasili vya kidini vinavyohusu asili na hatima ya mwanadamu katika jamii ya Waswahili ambapo mipaka baina ya dunia halisi na ile ya kifantasia na wahusika halisi na wale wakifantasia inavunjwa.

Author Biographies

Ahmad Kipacha

 Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela  

Hadija Jilala

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

Downloads

Published

2026-01-29